Koreshi Anatoa Amri ya Kurudishwa kwa Wayahudi
536 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Koreshi mfalme wa Uajemi, ili kulitimiza neno la Bwana lililosemwa na nabii Yeremia, Bwana aliusukuma moyo wa Koreshi mfalme wa Uajemi kutangaza katika himaya yake yote kwa maandishi:
2 “Hili ndilo asemalo Koreshi mfalme wa Uajemi:
“ ‘Bwana, Mungu wa mbinguni, amenipa falme zote duniani, na ameniagiza kumjengea Hekalu huko Yerusalemu katika Yuda. 3 Yeyote wa watu wake miongoni mwenu, Mungu wake na awe pamoja naye, wacha apande kwenda Yerusalemu katika Yuda na kujenga Hekalu la Bwana, Mungu wa Israeli, Mungu aliyeko huko Yerusalemu. 4 Nao watu wa mahali popote wale walionusurika wanapoishi sasa, watu hao wampe fedha na dhahabu, pamoja na vifaa na mifugo, mbali na sadaka za hiari kwa ajili ya Hekalu la Mungu huko Yerusalemu.’ ”
Wimbo wa kwenda juu.
1 Bwana alipowarejeza mateka Sayuni,
tulikuwa kama watu walioota ndoto.
2 Vinywa vyetu vilijaa kicheko,
ndimi zetu zilijaa nyimbo za shangwe.
Ndipo iliposemwa miongoni mwa mataifa,
“Bwana amewatendea mambo makuu.”
3 Bwana ametutendea mambo makuu,
nasi tumejaa furaha.
4 Ee Bwana, turejeshee watu wetu waliotekwa,
kama vijito katika Negebu.
5 Wapandao kwa machozi
watavuna kwa nyimbo za shangwe.
6 Yeye azichukuaye mbegu zake
kwenda kupanda, huku akilia,
atarudi kwa nyimbo za shangwe,
akichukua miganda ya mavuno yake.
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya wana wa Kora.
1 Ee Bwana, ulionyesha wema kwa nchi yako.
Ulimrejeshea Yakobo baraka zake.
2 Ulisamehe uovu wa watu wako,
na kufunika dhambi zao zote.
3 Uliweka kando ghadhabu yako yote
na umegeuka na kuiacha hasira yako kali.
4 Ee Mungu Mwokozi wetu, uturejeshe tena,
nawe uiondoe chuki yako juu yetu.
5 Je, utatukasirikia milele?
Utaendeleza hasira yako kwa vizazi vyote?
6 Je, hutatuhuisha tena,
ili watu wako wakufurahie?
7 Utuonyeshe upendo wako usiokoma, Ee Bwana,
utupe wokovu wako.
8 Nitasikiliza lile atakalosema Mungu aliye Bwana;
anaahidi amani kwa watu wake, watakatifu wake:
lakini nao wasirudie upumbavu.
9 Hakika wokovu wake uko karibu na wale wamchao,
ili utukufu wake udumu katika nchi yetu.
10 Upendo na uaminifu hukutana pamoja,
haki na amani hubusiana.
11 Uaminifu huchipua kutoka nchi,
haki hutazama chini kutoka mbinguni.
12 Naam, hakika Bwana atatoa kilicho chema,
nayo nchi yetu itazaa mavuno yake.
13 Haki itatangulia mbele yake
na kutengeneza njia kwa ajili ya hatua zake.
22 Katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Koreshi mfalme wa Uajemi, ili kulitimiza neno la Bwana lililosemwa na nabii Yeremia, Bwana aliusukuma moyo wa Koreshi mfalme wa Uajemi kutangaza katika himaya yake yote kwa maandishi:
23 “Hili ndilo asemalo Koreshi mfalme wa Uajemi:
“ ‘Bwana, Mungu wa mbinguni, amenipa falme zote duniani, na ameniagiza kumjengea Hekalu huko Yerusalemu katika Yuda. Yeyote wa watu wake miongoni mwenu, Mungu wake na awe pamoja naye, wacha huyo mtu na apande.’ ”