Balaamu na Balaki (continued)

1451 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Hesabu 24

1 Basi Balaamu alipoona imempendeza Bwana kubariki Israeli, hakuendelea tena kutafuta uchawi kama nyakati nyingine, bali aligeuza uso wake kuelekea nyikani. 2 Balaamu alipotazama nje na kuona Israeli amepiga kambi kabila kwa kabila, Roho wa Mungu akawa juu yake, 3 naye akatoa ujumbe wake:

“Ujumbe wa Balaamu mwana wa Beori,

ujumbe wake yeye ambaye jicho lake linaona vizuri;

4 ujumbe wake yeye ambaye husikia maneno ya Mungu,

ambaye huona maono kutoka kwa Mwenyezi,

ambaye huanguka kifudifudi, na ambaye macho yake yamefunguka:

5 “Tazama jinsi yalivyo mazuri mahema yako, ee Yakobo,

maskani yako, ee Israeli!

6 “Kama mabonde, yanaenea,

kama bustani kando ya mto,

kama miti ya udi iliyopandwa na Bwana,

kama mierezi kando ya maji.

7 Maji yatatiririka kutoka ndoo zake;

mbegu yake itakuwa na maji tele.

“Mfalme wake atakuwa mkuu kuliko Mfalme Agagi;

ufalme wake utatukuka.

8 “Mungu alimleta kutoka Misri;

yeye ana nguvu kama nyati.

Anayararua mataifa yaliyo adui zake,

na kuvunja mifupa yao vipande vipande;

huwachoma kwa mishale yake.

9 Hujikunyata na kuvizia kama simba,

kama simba jike; nani anayethubutu kumwamsha?

“Abarikiwe kila akubarikiye,

na alaaniwe kila akulaaniye!”

10 Ndipo hasira ya Balaki ikawaka dhidi ya Balaamu. Akapiga mikono yake pamoja, akamwambia Balaamu, “Nilikuita uje kuwalaani adui zangu, lakini umewabariki mara hizi tatu. 11 Sasa ondoka upesi uende nyumbani! Mimi nilisema nitakuzawadia vizuri sana, lakini Bwana amekuzuia usizawadiwe.”

12 Balaamu akamwambia Balaki, “Je, hukumbuki jinsi nilivyowaambia wajumbe uliowatuma kwangu? Niliwaambia hivi, 13 ‘Hata ikiwa Balaki angenipa jumba lake la kifalme likiwa limejazwa fedha na dhahabu, nisingeweza kufanya kitu chochote kwa matakwa yangu, kikiwa kizuri au kibaya, kwenda kinyume na agizo la Bwana, nami imenipasa kusema tu kile Bwana atakachosema’? 14 Sasa ninarudi kwa watu wangu. Lakini njoo, nikuonye kuhusu kile watu hawa watakachowatenda watu wako siku zijazo.”

15 Kisha Balaamu akatoa ujumbe wake:

“Ujumbe wa Balaamu mwana wa Beori,

ujumbe wake yeye ambaye jicho lake linaona vizuri;

16 ujumbe wake yeye ambaye husikia maneno ya Mungu,

ambaye ana maarifa kutoka kwa Aliye Juu Sana,

huona maono kutoka Mwenyezi,

ambaye huanguka kifudifudi

na ambaye macho yake yamefunguka:

17 “Namwona yeye, lakini si sasa;

namtazama yeye, lakini si karibu.

Nyota itatoka kwa Yakobo,

fimbo ya ufalme itainuka kutoka kwa Israeli.

Atawaponda Wamoabu vipaji vya nyuso

na mafuvu yote ya wana wa Shethi.

18 Edomu itamilikiwa,

Seiri, adui wake, itamilikiwa,

lakini Israeli atakuwa na nguvu.

19 Mtawala atakuja kutoka kwa Yakobo

na kuangamiza walionusurika katika mji.”

20 Kisha Balaamu akawaona watu wa Amaleki, na kutoa ujumbe wake:

“Amaleki ilikuwa ya kwanza miongoni mwa mataifa,

lakini mwisho wake itaangamizwa milele.”

21 Kisha akawaona Wakeni, akatoa ujumbe wake:

“Makao yenu ni salama,

kiota chenu kiko kwenye mwamba.

22 Hata hivyo ninyi Wakeni mtaangamizwa

Ashuru atakapowachukua mateka.”

23 Ndipo akatoa ujumbe wake:

“Lo, ni nani atakayeweza kuishi wakati Mungu atakapofanya hili?

24 Meli zitakuja kutoka pwani za Kitimu,

zitaitiisha Ashuru na Eberi,

lakini nao pia wataangamizwa.”

25 Kisha Balaamu akainuka na kurudi nyumbani kwake, naye Balaki akashika njia yake.

Safari ya Arobaini na Mbili: Nyanda za Moabu

Safari ya arobaini na mbili: nyanda za Moabu, kambi ikiwa kando ya Beth-Yeshimothi na Abel-Shitimu.

Hesabu 33:49

49 Huko kwenye tambarare za Moabu walipiga kambi kandokando ya Mto Yordani, kuanzia Beth-Yeshimothi mpaka Abel-Shitimu.

Ibada ya Sanamu ya Baali wa Peori

Hesabu 25

1 Israeli alipokuwa akikaa Shitimu, wanaume wa Israeli walianza kuzini na wanawake wa Kimoabu, 2 ambao waliwaalika kushiriki katika kutoa kafara kwa miungu yao. Watu wakala na kusujudu mbele ya miungu hii. 3 Kwa hiyo Israeli akaungana katika kumwabudu Baali wa Peori. Hasira ya Bwana ikawaka dhidi yao.

4 Bwana akamwambia Mose, “Uwachukue viongozi wote wa watu hawa, uwaue na uwaweke hadharani mchana peupe mbele za Bwana, ili hasira kali ya Bwana iweze kuondoka kwa Israeli.”

5 Kwa hiyo Mose akawaambia waamuzi wa Israeli, “Kila mmoja wenu lazima awaue wale wanaume wenu, walioshiriki katika kumwabudu Baali wa Peori.”

6 Ndipo mwanaume wa Kiisraeli akamleta mwanamke wa Kimidiani katika jamaa yake palepale mbele ya Mose na mkutano wote wa Israeli walipokuwa wakilia kwenye lango la Hema la Kukutania. 7 Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa kuhani Aroni, alipoona jambo hili, akaondoka kwenye kusanyiko, akachukua mkuki mkononi mwake, 8 akamfuata yule Mwisraeli ndani ya hema. Akawachoma mkuki wote wawili kwa pamoja, ukapenya kwenye mwili wa yule Mwisraeli na mwili wa yule mwanamke. Ndipo tauni iliyokuwepo dhidi ya Waisraeli ikakoma. 9 Lakini wale waliokufa kwa hiyo tauni walikuwa watu 24,000.

10 Bwana akamwambia Mose, 11 “Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa kuhani Aroni, amegeuza hasira yangu mbali na Waisraeli, kwa sababu alikuwa na wivu kama nilio nao kwa heshima yangu miongoni mwao, hata kwamba kwa wivu wangu sikuwaangamiza. 12 Kwa hiyo mwambie Finehasi ninafanya Agano langu la amani naye. 13 Yeye pamoja na wazao wake watakuwa na Agano la ukuhani milele, kwa sababu alikuwa na wivu kwa ajili ya heshima ya Mungu wake, na akafanya upatanisho kwa Waisraeli.”

14 Jina la Mwisraeli ambaye aliuawa pamoja na mwanamke wa Kimidiani ni Zimri mwana wa Salu, kiongozi wa jamaa ya Simeoni. 15 Jina la mwanamke wa Kimidiani aliyeuawa ni Kozbi binti wa Suri, aliyekuwa mkuu wa kabila la jamaa ya Wamidiani.

16 Bwana akamwambia Mose, 17 “Watendeeni Wamidiani kama adui na mwaue, 18 kwa sababu wao waliwatendea kama adui wakati waliwadanganya katika tukio la Peori na dada yao Kozbi, binti wa kiongozi wa Kimidiani, mwanamke ambaye aliuawa wakati tauni ilikuja kama matokeo ya tukio la Peori.”