Wakati wa Kuwekwa Wakfu kwa Hekalu la Solomoni

1004 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Zaburi 135–136

1 Msifuni Bwana.

Lisifuni jina la Bwana,

msifuni, enyi watumishi wa Bwana,

2 ninyi ambao mnatumika ndani ya nyumba ya Bwana,

katika nyua za nyumba ya Mungu wetu.

3 Msifuni Bwana, kwa kuwa Bwana ni mwema,

liimbieni sifa jina lake, kwa maana hilo lapendeza.

4 Kwa maana Bwana amemchagua Yakobo kuwa wake mwenyewe,

Israeli kuwa mali yake ya thamani.

5 Ninajua ya kuwa Bwana ni mkuu,

kwamba Bwana wetu ni mkuu kuliko miungu yote.

6 Bwana hufanya lolote apendalo,

mbinguni na duniani,

katika bahari na vilindi vyake vyote.

7 Hufanya mawingu kupanda kutoka miisho ya dunia;

hupeleka umeme wa radi pamoja na mvua

na huleta upepo kutoka ghala zake.

8 Alimuua mzaliwa wa kwanza wa Misri,

mzaliwa wa kwanza wa wanadamu na wanyama.

9 Alipeleka ishara zake na maajabu katikati yako, ee Misri,

dhidi ya Farao na watumishi wake wote.

10 Aliyapiga mataifa mengi,

na akaua wafalme wenye nguvu:

11 Mfalme Sihoni na Waamori,

Ogu mfalme wa Bashani

na wafalme wote wa Kanaani:

12 akatoa nchi yao kuwa urithi,

urithi kwa watu wake Israeli.

13 Ee Bwana, jina lako ladumu milele,

kumbukumbu za fahari zako, Ee Bwana, kwa vizazi vyote.

14 Maana Bwana atawathibitisha watu wake,

na kuwahurumia watumishi wake.

15 Sanamu za mataifa ni fedha na dhahabu,

zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu.

16 Zina vinywa, lakini haziwezi kusema,

zina macho, lakini haziwezi kuona;

17 zina masikio, lakini haziwezi kusikia,

wala hakuna pumzi katika vinywa vyao.

18 Wale wanaozitengeneza watafanana nazo,

vivyo hivyo wale wote wanaozitumainia.

19 Ee nyumba ya Israeli, msifuni Bwana;

ee nyumba ya Aroni, msifuni Bwana;

20 ee nyumba ya Lawi, msifuni Bwana;

ninyi mnaomcha, msifuni Bwana.

21 Msifuni Bwana kutoka Sayuni,

msifuni yeye aishiye Yerusalemu.

Msifuni Bwana.

136:1 Mshukuruni Bwana, kwa kuwa ni mwema.

Fadhili zake zadumu milele.

2 Mshukuruni Mungu wa miungu.

Fadhili zake zadumu milele.

3 Mshukuruni Bwana wa mabwana:

Fadhili zake zadumu milele.

4 Kwake yeye pekee atendaye maajabu makuu,

Fadhili zake zadumu milele.

5 Ambaye kwa ufahamu wake aliziumba mbingu,

Fadhili zake zadumu milele.

6 Ambaye aliitandaza dunia juu ya maji,

Fadhili zake zadumu milele.

7 Ambaye aliumba mianga mikubwa,

Fadhili zake zadumu milele.

8 Jua litawale mchana,

Fadhili zake zadumu milele.

9 Mwezi na nyota vitawale usiku,

Fadhili zake zadumu milele.

10 Kwake yeye aliyemuua mzaliwa wa kwanza wa Misri,

Fadhili zake zadumu milele.

11 Na kuwatoa Israeli katikati yao,

Fadhili zake zadumu milele.

12 Kwa mkono wenye nguvu ulionyooshwa,

Fadhili zake zadumu milele.

13 Kwake yeye aliyeigawa Bahari ya Shamu,

Fadhili zake zadumu milele.

14 Na kuwapitisha Israeli katikati yake,

Fadhili zake zadumu milele.

15 Lakini alimfagia Farao na jeshi lake katika Bahari ya Shamu,

Fadhili zake zadumu milele.

16 Kwake yeye aliyewaongoza watu wake katika jangwa,

Fadhili zake zadumu milele.

17 Ambaye aliwapiga wafalme wenye nguvu,

Fadhili zake zadumu milele.

18 Naye aliwaua wafalme wenye nguvu,

Fadhili zake zadumu milele.

19 Sihoni mfalme wa Waamori,

Fadhili zake zadumu milele.

20 Ogu mfalme wa Bashani,

Fadhili zake zadumu milele.

21 Akatoa nchi yao kuwa urithi,

Fadhili zake zadumu milele.

22 Urithi kwa Israeli mtumishi wake,

Fadhili zake zadumu milele.

23 Aliyetukumbuka katika unyonge wetu,

Fadhili zake zadumu milele.

24 Alituweka huru toka adui zetu,

Fadhili zake zadumu milele.

25 Ambaye humpa chakula kila kiumbe.

Fadhili zake zadumu milele.

26 Mshukuruni Mungu wa mbinguni,

Fadhili zake zadumu milele.