Utangulizi wa Kuangamizwa kwa Yerusalemu

Utangulizi wa jumla wa simulizi la kuangamizwa kwa hekalu na Yerusalemu.

595 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Nyakati 36:11–21

11 Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka kumi na mmoja. 12 Alifanya maovu machoni pa Bwana Mungu wake, wala hakujinyenyekeza mbele ya nabii Yeremia, ambaye alinena neno la Bwana. 13 Pia alimwasi Mfalme Nebukadneza, ambaye alikuwa amemwapisha kwa jina la Mungu. Akashupaza shingo na akafanya moyo wake kuwa mgumu wala hakutaka kumgeukia Bwana, Mungu wa Israeli. 14 Zaidi ya hayo viongozi wote wa makuhani pamoja na watu wakazidi kukosa uaminifu zaidi na zaidi, wakafanya machukizo yote kama walivyofanya mataifa wakinajisi Hekalu la Bwana alilokuwa amelitakasa huko Yerusalemu.

15 Bwana, Mungu wa baba zao, akawapelekea neno kupitia wajumbe wake tena na tena, kwa sababu alikuwa anawahurumia watu wake pamoja na mahali pa maskani yake. 16 Lakini waliwadhihaki wajumbe wa Bwana wakayadharau maneno yake na kuwacheka manabii wake mpaka ghadhabu ya Bwana ikawa kubwa dhidi ya watu wake na hakukuwa na namna ya kuituliza. 17 Mungu akamwinua dhidi yao mfalme wa Wakaldayo, aliyewaua vijana wao wa kiume kwa upanga ndani ya mahali patakatifu, ambaye hakumbakiza kijana mwanaume wala kijana mwanamke, wazee wala vikongwe. Mungu akawatia wote mikononi mwa Nebukadneza. 18 Akavichukua kwenda Babeli vyombo vyote kutoka Hekalu la Mungu, vikubwa na vidogo, hazina za Hekalu la Bwana pamoja na hazina za mfalme na za maafisa wake. 19 Wakalichoma Hekalu la Mungu na kuzibomoa kuta za Yerusalemu, wakachoma moto majumba yote ya kifalme na kuharibu kila kitu chake cha thamani.

20 Wale watu walionusurika kuuawa kwa upanga wakachukuliwa kwenda uhamishoni Babeli. Nao wakawa watumishi wake na wa wanawe mpaka wakati wa utawala wa ufalme wa Uajemi ulifika. 21 Nchi ikaendelea kufurahia pumziko lake la Sabato, wakati wote wa kufanywa kwake ukiwa ilipumzika mpaka ile miaka sabini ilipotimia katika kutimiza neno la Bwana lililonenwa na Yeremia.

2 Wafalme 25:1–2

1 Hivyo katika mwaka wa tisa wa utawala wa Sedekia, katika siku ya kumi ya mwezi wa kumi, Nebukadneza mfalme wa Babeli, akiwa na jeshi lake lote, alifanya vita dhidi ya Yerusalemu. Akapiga kambi nje ya mji na kuuzunguka mji pande zote. 2 Mji ulizungukwa na jeshi mpaka mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Mfalme Sedekia.

Wakaldayo Wanakaribia; Watumwa wa Jamii ya Mwebrania Wanaachiliwa Huru 590 KK

Jeshi la Wakaldayo linakaribia. Kukamatwa kwa Sedekia na kutekwa kwa mji kunatabiriwa. Watumwa wa jamii ya Mwebrania wanaachiliwa huru.

Yeremia 39:1

1 Hivi ndivyo Yerusalemu ilivyotwaliwa: Katika mwaka wa tisa wa utawala wa Mfalme Sedekia wa Yuda, katika mwezi wa kumi, Nebukadneza mfalme wa Babeli akiwa na jeshi lake lote alifanya vita dhidi ya Yerusalemu na akauzunguka mji.

Yeremia 37:1–4

1 Sedekia mwana wa Yosia akafanywa kuwa mfalme wa Yuda na Nebukadneza mfalme wa Babeli, naye akatawala mahali pa Yehoyakini mwana wa Yehoyakimu. 2 Lakini sio Sedekia, wala watumishi wake, wala watu wa nchi walisikiliza maneno ya Bwana aliyonena kupitia kwa nabii Yeremia.

3 Hata hivyo, Mfalme Sedekia akamtuma Yehukali mwana wa Shelemia, pamoja na kuhani Sefania mwana wa Maaseya kwa nabii Yeremia na ujumbe huu: “Tafadhali utuombee kwa Bwana, Mungu wetu.”

4 Wakati huu Yeremia alikuwa huru kuingia na kutoka katikati ya watu, kwa sababu alikuwa bado hajatiwa gerezani.

Yeremia 34:1–10

1 Wakati Nebukadneza mfalme wa Babeli na jeshi lake lote, pamoja na falme zote na mataifa katika himaya aliyotawala walipokuwa wakipigana dhidi ya Yerusalemu pamoja na miji yote inayoizunguka, neno hili lilimjia Yeremia kutoka kwa Bwana: 2 “Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli, kusema: Nenda kwa Sedekia mfalme wa Yuda umwambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Ninakaribia kuutia mji huu mikononi mwa mfalme wa Babeli, naye atauteketeza kwa moto. 3 Hutaweza kuepuka mkono wake, bali hakika utatekwa na kukabidhiwa kwake. Utamwona mfalme wa Babeli kwa macho yako mwenyewe, naye atazungumza nawe ana kwa ana. Nawe utakwenda Babeli.

4 “ ‘Lakini sikia ahadi ya Bwana, ee Sedekia mfalme wa Yuda. Hili ndilo asemalo Bwana kukuhusu: Hutakufa kwa upanga, 5 utakufa kwa amani. Kama vile watu walivyowasha moto wa maziko kwa heshima ya baba zako, wafalme waliokutangulia, ndivyo watu watakavyowasha moto kwa heshima yako na kuomboleza, wakisema: “Ole, Ee Bwana!” Mimi mwenyewe ninaweka ahadi hii, asema Bwana.’ ”

6 Ndipo nabii Yeremia akamwambia Sedekia mfalme wa Yuda mambo haya yote huko Yerusalemu, 7 wakati jeshi la mfalme wa Babeli lilipokuwa likipigana dhidi ya Yerusalemu na miji mingine ya Yuda ambayo bado ilikuwa imara, yaani Lakishi na Azeka. Hii ilikuwa miji pekee yenye ngome iliyobaki katika Yuda.

8 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Bwana, baada ya Mfalme Sedekia kufanya agano na watu wote huko Yerusalemu ili kutangaza uhuru kwa watumwa. 9 Kila mmoja alipaswa kuwaacha huru watumwa wake wa Kiebrania, wanawake na wanaume. Hakuna yeyote aliyeruhusiwa kumshikilia Myahudi mwenzake kama mtumwa. 10 Kwa hiyo maafisa wote na watu walioingia katika agano hili wakakubali kwamba watawaacha huru watumwa wao wa kiume na wa kike, na hawatawashikilia tena kama watumwa. Wakakubali na wakawaacha huru.