Amosi Anatabiri dhidi ya Mataifa na Israeli (continued)
Amosi anatangaza hukumu dhidi ya mataifa jirani, na dhidi ya Israeli na Yuda.
793 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Sikia neno hili, ee nyumba ya Israeli, ombolezo hili ninalifanya kuwahusu ninyi:
2 “Bikira Israeli ameanguka,
kamwe hatainuka tena,
ameachwa pweke katika nchi yake,
hakuna yeyote wa kumwinua.”
3 Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:
“Wakati mmoja wa miji yako utakapopeleka watu elfu moja vitani kwa ajili ya Israeli,
mia moja tu watarudi;
wakati mji utakapopeleka mia moja,
kumi tu ndio watarudi hai.”
4 Hili ndilo Bwana asemalo kwa nyumba ya Israeli:
“Nitafuteni mpate kuishi;
5 msitafute Betheli,
msiende Gilgali,
msisafiri kwenda Beer-Sheba.
Kwa maana kwa hakika Gilgali itakwenda uhamishoni,
na Betheli itafanywa kuwa si kitu.”
6 Mtafuteni Bwana mpate kuishi,
au atafagia nyumba ya Yosefu kama moto;
utawateketeza, nayo Betheli
haitakuwa na yeyote wa kuuzima.
7 Ninyi ambao mnageuza haki kuwa uchungu
na kuiangusha haki chini
8 (yeye ambaye alifanya Kilimia na Orioni,
ambaye hugeuza giza kuwa mapambazuko
na mchana kuwa usiku,
ambaye huyaita maji ya bahari
na kuyamwaga juu ya uso wa nchi:
Bwana ndilo jina lake;
9 yeye hufanya maangamizo kwenye ngome
na kufanya mji uliozungushiwa ngome kuwa ukiwa),
10 mnamchukia yule akemeaye mahakamani,
na kumdharau yule ambaye husema kweli.
11 Mnamgandamiza maskini
na kumlazimisha awape nafaka.
Kwa hiyo, ingawa mmejenga majumba ya mawe ya fahari,
hamtaishi ndani yake;
ingawa mmepanda mashamba mazuri ya mizabibu,
hamtakunywa divai yake.
12 Kwa kuwa ninajua hesabu ya makosa yenu
na ukubwa wa dhambi zenu.
Mmewaonea wenye haki na kupokea rushwa
na kuzuia haki ya maskini mahakamani.
13 Kwa hiyo mtu mwenye busara hunyamaza kimya nyakati kama hizo,
kwa kuwa nyakati ni mbaya.
14 Tafuteni mema, wala si mabaya,
ili mpate kuishi.
Ndipo Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote atakuwa pamoja nanyi,
kama msemavyo yupo nanyi.
15 Yachukieni maovu, yapendeni mema;
dumisheni haki mahakamani.
Yamkini Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote
atawahurumia mabaki ya Yosefu.
16 Kwa hiyo hili ndilo Bwana, Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote, asemalo:
“Kutakuwepo maombolezo katika barabara zote
na vilio vya uchungu katika njia kuu zote.
Wakulima wataitwa kuja kulia,
na waombolezaji waje kuomboleza.
17 Kutakuwepo kuomboleza katika mashamba yote ya mizabibu,
kwa kuwa nitapita katikati yenu,”
asema Bwana.
18 Ole wenu ninyi mnaoitamani
siku ya Bwana!
Kwa nini mnaitamani siku ya Bwana?
Siku hiyo itakuwa giza, si nuru.
19 Itakuwa kama vile mtu aliyemkimbia simba
kumbe akakutana na dubu,
kama vile mtu aliyeingia nyumbani mwake
na kuupumzisha mkono wake kwenye ukuta,
kumbe akaumwa na nyoka.
20 Je, siku ya Bwana haitakuwa giza, na si nuru:
giza nene, bila mwonzi wa mwanga?
21 “Ninachukia, ninazidharau sikukuu zenu za dini;
siwezi kuvumilia makusanyiko yenu.
22 Hata ingawa mnaniletea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka za nafaka,
sitazikubali.
Ingawa mnaniletea sadaka nzuri za amani,
sitazitambua.
23 Niondoleeni kelele za nyimbo zenu!
Sitasikiliza sauti za vinubi vyenu.
24 Lakini acheni haki itiririke kama mto,
na uadilifu uwe kama kijito kisichokauka!
25 “Je, mliniletea dhabihu na sadaka
kwa miaka arobaini kule jangwani,
ee nyumba ya Israeli?
26 Mmeyainua madhabahu ya mfalme wenu,
Sikuthi mungu wenu mtawala,
na Kiuni mungu wenu wa nyota,
ambao mliwatengeneza wenyewe.
27 Kwa sababu hiyo nitawapeleka uhamishoni mbali kupita Dameski,”
asema Bwana, ambaye jina lake ni Mungu Mwenye Nguvu Zote.
6:1 Ole wenu ninyi mnaostarehe na kuridhika katika Sayuni,
na ninyi mnaojisikia salama juu ya Mlima Samaria,
ninyi watu mashuhuri wa taifa lililoendelea kuliko mataifa mengine,
ambao watu wa Israeli wanawategemea!
2 Nendeni Kalne mkaone kutoka huko;
mwende hadi Hamathi iliyo kuu,
kisha mshuke hadi Gathi ya Wafilisti.
Je, wao ni bora kuliko falme zenu mbili?
Je, nchi yao ni kubwa kuliko yenu?
3 Mnaiweka mbali siku iliyo mbaya
na kuleta karibu utawala wa kuogofya.
4 Ninyi mnalala juu ya vitanda vilivyofunikwa kwa pembe za ndovu,
na kujinyoosha juu ya viti vya fahari.
Mnajilisha kwa wana-kondoo wazuri
na ndama walionenepeshwa.
5 Ninyi mnapiga vinubi kama Daudi,
huku mkitunga nyimbo za vinanda mbalimbali.
6 Mnakunywa mvinyo kwa bakuli zilizojazwa,
na mnajipaka mafuta mazuri,
lakini hamhuzuniki kwa maangamizi ya Yosefu.
7 Kwa hiyo mtakuwa miongoni mwa watu wa kwanza kwenda uhamishoni;
karamu zenu na kustarehe kutakoma.
8 Bwana Mwenyezi ameapa kwa nafsi yake mwenyewe: Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote asema:
“Nachukia kiburi cha Yakobo,
nachukia ngome zake;
nitautoa mji wao na kila kitu
kilichomo ndani mwake.”
9 Kama watu kumi watabaki katika nyumba moja, wao pia watakufa. 10 Kama jamaa ambaye atachoma miili akija ili kuitoa nje ya nyumba, na kumuuliza yeyote ambaye bado anajificha humo, “Je, yuko mtu yeyote pamoja nawe?” Naye akisema, “Hapana,” ndipo atakaposema, “Nyamaza kimya! Haturuhusiwi kutaja jina la Bwana.”
11 Kwa kuwa Bwana ameamuru,
naye atabomoa jumba kubwa vipande vipande
na nyumba ndogo vipande vidogo vidogo.
12 Je, farasi waweza kukimbia kwenye miamba mikali?
Je, aweza mtu kulima huko kwa maksai?
Lakini mmegeuza haki kuwa sumu
na matunda ya uadilifu kuwa uchungu:
13 ninyi mnaoshangilia kushindwa kwa Lo-Debari
na kusema, “Je, hatukuteka Karnaimu kwa nguvu zetu wenyewe?”
14 Maana Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote asema,
“Nitainua taifa dhidi yenu, ee nyumba ya Israeli,
nalo litawatesa kuanzia Lebo-Hamathi
hadi Bonde la Araba.”
7:1 Hili ndilo alilonionyesha Bwana Mwenyezi katika maono: Alikuwa anaandaa makundi ya nzige baada ya kuvunwa fungu la mfalme na wakati ule tu mimea ya pili ilipokuwa ikichipua. 2 Wakati nzige walikuwa wamekula mimea yote ya nchi, nililia kwa sauti kuu, “Bwana Mwenyezi, samehe! Je, Yakobo atawezaje kuendelea kuishi? Yeye ni mdogo sana!”
3 Kwa hiyo Bwana akaghairi.
Kisha Bwana akasema, “Hili halitatokea.”
4 Hili ndilo Bwana Mwenyezi alilonionyesha katika maono: Bwana Mwenyezi alikuwa akiita hukumu ya moto; nao ulikausha vilindi vikuu, ukateketeza nchi. 5 Ndipo nikalia, “Bwana Mwenyezi, nakusihi, zuia! Je, Yakobo atawezaje kuendelea kuishi? Yeye ni mdogo sana!”
6 Kwa hiyo Bwana akaghairi.
Bwana Mwenyezi akasema, “Hili nalo halitatokea.”
7 Hili ndilo alilonionyesha katika maono: Bwana alikuwa amesimama karibu na ukuta ambao ulikuwa umejengwa kwa timazi, akiwa na uzi wa timazi mkononi mwake. 8 Naye Bwana akaniuliza, “Je, Amosi unaona nini?”
Nikamjibu, “Uzi wa timazi.”
Kisha Bwana akasema, “Tazama, ninaweka uzi wa timazi miongoni mwa watu wangu Israeli; sitawahurumia tena.
9 “Mahali pa Isaki pa juu pa kuabudia miungu pataangamizwa,
na mahali patakatifu pa Israeli pa kuabudia pataharibiwa;
kwa upanga wangu nitainuka
dhidi ya nyumba ya Yeroboamu.”