Abrahamu Anamwoa Ketura
1856 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Abrahamu alioa mke mwingine, ambaye jina lake aliitwa Ketura. 2 Huyu alimzalia Zimrani, Yokshani, Medani, Midiani, Ishbaki na Shua. 3 Yokshani alikuwa baba wa Sheba na Dedani, wazao wa Dedani walikuwa Waashuri, Waletushi na Waleumi. 4 Wana wa Midiani walikuwa Efa, Eferi, Hanoki, Abida na Eldaa. Hawa wote walikuwa uzao wa Ketura.
5 Abrahamu akamwachia Isaki kila kitu alichokuwa nacho. 6 Lakini Abrahamu alipokuwa bado hai, akawapa watoto wa masuria wake zawadi, kisha akawaondoa waende kuishi pande za mashariki mbali na mwanawe Isaki.
Kuzaliwa kwa Esau na Yakobo 1836 KK
19 Hivi ndivyo vizazi vya Isaki mwana wa Abrahamu.
Abrahamu akamzaa Isaki, 20 Isaki alikuwa na umri wa miaka arobaini alipomwoa Rebeka binti Bethueli Mwaramu kutoka Padan-Aramu, nduguye Labani Mwaramu.
21 Isaki akamwomba Bwana kwa ajili ya mke wake, kwa sababu alikuwa tasa. Bwana akajibu maombi yake na Rebeka mkewe akapata mimba. 22 Watoto wakashindana tumboni mwake, akasema, “Kwa nini haya yanatokea kwangu?” Kwa hiyo akaenda kumuuliza Bwana.
23 Bwana akamjibu,
“Mataifa mawili yamo tumboni mwako,
na mataifa hayo mawili
kutoka ndani yako watatenganishwa.
Mmoja atakuwa na nguvu zaidi kuliko mwingine,
na yule mkubwa atamtumikia yule mdogo.”
24 Wakati wake wa kujifungua ulipotimia, walikuwepo mapacha wa kiume tumboni mwake. 25 Wa kwanza kuzaliwa alikuwa mwekundu, mwili wake wote ulikuwa kama mtu aliyevaa vazi lenye nywele; wakamwita jina lake Esau. 26 Baadaye, ndugu yake akatoka, mkono wake ukiwa umemshika Esau kisigino; akaitwa jina lake Yakobo. Isaki alikuwa mwenye miaka sitini Rebeka alipowazaa.
27 Watoto wakakua, naye Esau akakuwa mwindaji hodari, mtu wa mbugani, wakati Yakobo alikuwa mtu mtulivu, mwenye kukaa nyumbani. 28 Isaki, ambaye alikuwa anapendelea zaidi nyama za porini, alimpenda Esau, bali Rebeka alimpenda Yakobo.
Kifo cha Abrahamu 1821 KK
7 Kwa jumla, Abrahamu aliishi miaka 175. 8 Ndipo Abrahamu akapumua pumzi ya mwisho na akafa akiwa mwenye umri mzuri, mzee aliyeshiba siku, naye akakusanywa pamoja na watu wake. 9 Watoto wake Isaki na Ishmaeli wakamzika katika pango la Makpela karibu na Mamre, katika shamba lililokuwa la Efroni mwana wa Sohari Mhiti, 10 Shamba ambalo Abrahamu alilinunua kwa Wahiti. Hapo ndipo Abrahamu alipozikwa pamoja na mkewe Sara.