Aroni na Wanawe Wanawekwa Wakfu (continued)

Aroni na wanawe wanawekwa wakfu, pamoja na mambo mengine.

1491 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Kutoka 30–31

1 “Tengeneza madhabahu kwa mbao za mshita kwa ajili ya kufukizia uvumba. 2 Madhabahu hayo yawe mraba, urefu na upana wake dhiraa moja, na kimo cha dhiraa mbili, nazo pembe zake zitakuwa kitu kimoja nayo. 3 Funika hayo madhabahu juu na pande zote na pia pembe zake kwa dhahabu safi, na uifanyizie ukingo wa dhahabu kuizunguka. 4 Tengeneza pete mbili za dhahabu kwa ajili ya madhabahu chini ya huo ukingo, ziwe mbili kila upande, za kushikilia hiyo mipiko itumikayo kuibebea madhabahu. 5 Tengeneza mipiko kwa miti ya mshita na uifunike kwa dhahabu. 6 Weka hayo madhabahu mbele ya lile pazia lililo mbele ya Sanduku la Ushuhuda, lililo mbele ya kiti cha rehema kilicho juu ya Sanduku la Ushuhuda, mahali ambapo nitakutana nawe.

7 “Itampasa Aroni kufukiza uvumba wenye harufu nzuri juu ya madhabahu kila siku asubuhi wakati anapowasha zile taa. 8 Itampasa afukize uvumba tena wakati anapowasha taa wakati wa machweo ili uvumba ufukizwe daima mbele za Bwana kwa vizazi vijavyo. 9 Usifukize uvumba mwingine wowote juu ya madhabahu haya au sadaka nyingine yoyote ya kuteketezwa wala sadaka ya nafaka, wala usimimine sadaka ya kinywaji juu yake. 10 Mara moja kwa mwaka Aroni atafanya upatanisho juu ya pembe za hayo madhabahu. Upatanisho huu wa mwaka lazima ufanywe kwa damu ya sadaka ya upatanisho kwa ajili ya dhambi kwa vizazi vijavyo. Ni takatifu sana kwa Bwana.”

11 Naye Bwana akamwambia Mose, 12 “Utakapowahesabu Waisraeli, kila mmoja lazima alipe kwa Bwana fidia kwa ajili ya nafsi yake wakati wa kuhesabiwa kwake. Ndipo hakutakuwa na pigo juu yao unapowahesabu. 13 Kila mmoja anayekwenda upande wa wale waliokwisha hesabiwa atatoa nusu shekeli, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, ambayo ina uzito wa gera ishirini. Hii nusu shekeli ni sadaka kwa Bwana. 14 Wote wale wanaovuka, wenye umri wa miaka ishirini au zaidi, watatoa sadaka kwa Bwana. 15 Matajiri hawatalipa zaidi ya nusu shekeli, nao maskini hawatatoa pungufu wakati mnatoa sadaka kwa Bwana kwa kufanya upatanisho wa nafsi zenu. 16 Utapokea fedha ya upatanisho kutoka kwa Waisraeli na uzitumie kwa ajili ya huduma ya Hema la Kukutania. Itakuwa ni ukumbusho kwa Waisraeli mbele za Bwana kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu.”

17 Kisha Bwana akamwambia Mose, 18 “Tengeneza sinia la shaba lenye kitako cha shaba kwa ajili ya kunawia. Liweke kati ya Hema la Kukutania na madhabahu, kisha uweke maji ndani yake. 19 Aroni na wanawe watanawa mikono na miguu yao kwa maji yatokayo katika hilo sinia. 20 Wakati wowote wanapoingia katika Hema la Kukutania, watanawa kwa maji ili kwamba wasije wakafa. Pia, wanapokaribia madhabahu ili kuhudumu kwa kuleta sadaka zilizotolewa kwa Bwana kwa moto, 21 watanawa mikono na miguu yao ili kwamba wasije wakafa. Hii itakuwa ni amri ya kudumu kwa ajili ya Aroni na wazao wake kwa vizazi vijavyo.”

22 Kisha Bwana akamwambia Mose, 23 “Chukua vikolezi bora vifuatavyo: shekeli 500 za manemane ya maji, shekeli 250 za mdalasini wenye harufu nzuri, shekeli 250 za miwa yenye harufu nzuri, 24 shekeli 500 za aina nyingine ya mdalasini, vyote kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, pia hini ya mafuta ya zeituni. 25 Vitengeneze vikolezi hivi kuwa mafuta matakatifu ya upako yenye harufu nzuri, kazi ya mtengeneza manukato. Yatakuwa mafuta matakatifu ya upako. 26 Kisha yatumie kupaka hilo Hema la Kukutania, Sanduku la Ushuhuda, 27 meza na vifaa vyake vyote, kinara cha taa na vifaa vyake vyote, madhabahu ya kufukizia uvumba, 28 madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote na sinia pamoja na kitako chake. 29 Utaviweka wakfu ili viwe vitakatifu sana na kila kitakachoigusa kitakuwa kitakatifu.

30 “Mtie Aroni na wanawe mafuta na uwaweke wakfu ili waweze kunitumikia katika kazi ya ukuhani. 31 Waambie Waisraeli, ‘Haya yatakuwa mafuta matakatifu yangu ya upako kwa vizazi vijavyo. 32 Usiyamimine juu ya miili ya wanadamu wala usitengeneze mafuta ya aina nyingine kwa utaratibu huu. Ni mafuta matakatifu na ni lazima myaone kuwa ni matakatifu. 33 Mtu yeyote atakayetengeneza manukato kama hayo na yeyote atakayeyamimina juu ya mtu yeyote ambaye si kuhani atakatiliwa mbali na watu wake.’ ”

34 Kisha Bwana akamwambia Mose, “Chukua vikolezi vyenye harufu nzuri vifuatavyo: natafi, shekelethi, kelbena na uvumba safi vyote vikiwa na vipimo sawa, 35 pia tengeneza mchanganyiko wa uvumba wenye harufu nzuri, kazi ya mtengeneza manukato. Utiwe chumvi ili upate kuwa safi na mtakatifu. 36 Saga baadhi yake kuwa unga na uweke mbele ya Sanduku la Ushuhuda ndani ya Hema la Kukutania, mahali ambapo nitakutana nawe. Itakuwa takatifu sana kwenu. 37 Msitengeneze uvumba mwingine wowote wa namna hii kwa ajili yenu wenyewe; uoneni kuwa ni mtakatifu kwa Bwana. 38 Yeyote atakayetengeneza uvumba kama huu ili kufurahia harufu yake nzuri lazima akatiliwe mbali na watu wake.”

31:1 Ndipo Bwana akamwambia Mose, 2 “Tazama, nimemchagua Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda, 3 nami nimemjaza Roho wa Mungu, pamoja na ustadi, uwezo na ujuzi katika aina zote za ufundi, 4 ili kubuni michoro ya kupendeza katika ufundi wa dhahabu, fedha na shaba, 5 kuchonga vito na kuvitia mahali, kufanya ufundi kwa mbao, na kujishughulisha na aina zote za ufundi. 6 Tena nimemteua Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, ili kumsaidia. Pia mafundi wote nimewapa ustadi wa kutengeneza kila kitu nilichokuamuru wewe: 7 Hema la Kukutania, Sanduku la Ushuhuda pamoja na kiti cha rehema juu yake, pia na vifaa vyote vya kwenye hema, 8 meza na vifaa vyake, kinara cha taa cha dhahabu safi na vifaa vyake vyote, madhabahu ya kufukizia uvumba, 9 madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote, sinia na kinara chake, 10 pamoja na mavazi matakatifu yaliyofumwa ya kuhani Aroni, na mavazi kwa ajili ya wanawe wakati wanahudumu katika kazi ya ukuhani, 11 pia mafuta ya upako na uvumba wenye harufu nzuri kwa ajili ya Mahali Patakatifu. Watavitengeneza sawasawa kama vile nilivyokuagiza wewe.”

12 Kisha Bwana akamwambia Mose, 13 “Waambie Waisraeli, ‘Ninyi ni lazima mzishike Sabato zangu. Hii itakuwa ni ishara kati yangu na ninyi kwa ajili ya vizazi vijavyo, ili mpate kujua kwamba Mimi Ndimi Bwana, niwafanyaye ninyi watakatifu.

14 “ ‘Mtaishika Sabato, kwa sababu ni takatifu kwenu. Yeyote atakayeinajisi lazima auawe, yeyote atakayefanya kazi siku hiyo lazima akafie mbali na watu wake. 15 Kwa siku sita, mtafanya kazi, lakini siku ya saba ni Sabato ya kupumzika, takatifu kwa Bwana. Yeyote afanyaye kazi yoyote siku ya Sabato ni lazima auawe. 16 Waisraeli wataishika Sabato, kuiadhimisha kwa vizazi vijavyo kuwa Agano la milele. 17 Itakuwa ishara kati yangu na Waisraeli milele, kwa kuwa kwa muda wa siku sita Bwana aliumba mbingu na dunia, na siku ya saba akaacha kufanya kazi, akapumzika.’ ”

18 Bwana alipomaliza kusema na Mose juu ya Mlima Sinai, Mungu akampa vile vibao viwili vya Ushuhuda, vibao vya mawe vilivyoandikwa kwa kidole cha Mungu.