Ono la Ibada za Sanamu Zilizosababisha Uhamisho (continued)

Ono la ibada za sanamu zilizosababisha Uhamisho wa Babeli.

594 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Ezekieli 10:1–11:21

1 Nikatazama, nikaona juu ya ile nafasi iliyokuwa juu ya vichwa vya wale makerubi kulikuwa na kitu mfano wa kiti cha enzi cha yakuti samawi. 2 Bwana akamwambia mtu yule aliyekuwa amevaa nguo ya kitani, “Ingia katikati ya yale Magurudumu yaliyo chini ya makerubi. Ukaijaze mikono yako makaa ya mawe ya moto kutoka katikati ya makerubi na uyatawanye juu ya mji.” Nilipokuwa nikiangalia, akaingia ndani.

3 Basi wale makerubi walikuwa wamesimama upande wa kusini wa Hekalu wakati yule mtu alipoingia ndani, wingu likaujaza ule ukumbi wa ndani. 4 Kisha utukufu wa Bwana ukainuka kutoka juu ya wale makerubi ukaenda kwenye kizingiti cha Hekalu. Wingu likajaza Hekalu, nao ukumbi ukajawa na mngʼao wa utukufu wa Bwana. 5 Sauti ya mabawa ya wale makerubi ingeweza kusikika mpaka kwenye ukumbi wa nje, kama sauti ya Mungu Mwenyezi wakati anapoongea.

6 Bwana alipomwamuru yule mtu aliyevaa nguo za kitani akisema, “Chukua moto toka katikati ya magurudumu, kutoka katikati ya makerubi,” yule mtu aliingia ndani akasimama pembeni mwa gurudumu. 7 Ndipo mmoja wa wale makerubi akanyoosha mkono wake kwenye moto uliokuwa katikati yao. Akachukua baadhi ya moto na kuutia mikononi mwa yule mtu aliyevaa mavazi ya kitani, naye akaupokea akatoka nje. 8 (Chini ya mabawa ya makerubi paliweza kuonekana kitu kilichofanana na mikono ya mwanadamu.)

9 Nikatazama, nikaona magurudumu manne kando ya makerubi, moja kando ya kila kerubi. Magurudumu hayo yalimetameta kama kito cha zabarajadi. 10 Kule kuonekana kwake, yote manne yalifanana kila gurudumu lilikuwa kama linazunguka ndani ya lingine. 11 Yalipozunguka, yalikwenda kokote katika pande nne walikoelekea wale makerubi. Magurudumu hayakugeuka wakati makerubi yalipokwenda. Makerubi walikwenda upande wowote kichwa kilikoelekea pasipo kugeuka walipokuwa wakienda. 12 Miili yao yote, pamoja na migongo yao, mikono na mabawa yao yote yalikuwa yamejaa macho kabisa kama yalivyokuwa yale magurudumu yao manne. 13 Nikasikia magurudumu yakiitwa, “Magurudumu ya kisulisuli.” 14 Kila mmoja wa wale makerubi alikuwa na nyuso nne: Uso mmoja ulikuwa kama vile wa kerubi, uso wa pili ulikuwa wa mwanadamu, uso wa tatu ulikuwa wa simba na uso wa nne ulikuwa wa tai.

15 Kisha makerubi wakapaa juu. Hawa ndio wale viumbe walio hai niliowaona kando ya Mto Kebari. 16 Wakati makerubi walipokwenda, magurudumu yaliyoko kando yao yalikwenda na wakati makerubi walipotanda mabawa yao wapate kupaa juu kutoka ardhi, magurudumu yale hayakuondoka pembeni mwao. 17 Makerubi yaliposimama kimya, nayo pia yalitulia kimya, nao makerubi yalipoinuka juu, magurudumu nayo yaliinuka juu pamoja nao, kwa sababu roho ya vile viumbe hai ilikuwa ndani yake.

18 Kisha utukufu wa Bwana ukaondoka pale kwenye kizingiti cha Hekalu na kusimama juu ya wale makerubi. 19 Nilipokuwa nikitazama, makerubi yakatanda mabawa yao na kuinuka kutoka ardhini, nao walipokuwa wakienda, yale magurudumu yakaenda pamoja nao. Wakasimama kwenye ingilio la lango la mashariki la nyumba ya Bwana, nao utukufu wa Mungu wa Israeli ukawa juu yao.

20 Hawa walikuwa ndio viumbe hai niliokuwa nimewaona chini ya Mungu wa Israeli kando ya Mto Kebari, nami nikatambua ya kuwa hao walikuwa makerubi. 21 Kila mmoja alikuwa na nyuso nne, mabawa manne, chini ya mabawa yao kulikuwa na kile kilichoonekana kama mikono ya mwanadamu. 22 Nyuso zao zilifanana kama zile nilizokuwa nimeziona kando ya Mto Kebari. Kila mmoja alikwenda mbele moja kwa moja.

11:1 Ndipo Roho akaniinua na kunileta mpaka kwenye lango la nyumba ya Bwana linalotazama upande wa mashariki. Pale kwenye ingilio la lango kulikuwepo wanaume ishirini na watano, nami nikaona miongoni mwao Yaazania mwana wa Azuri na Pelatia mwana wa Benaya, viongozi wa watu. 2 Bwana akaniambia, “Mwanadamu, hawa ndio wafanyao hila na kutoa mashauri potovu katika mji huu. 3 Wao husema, ‘Je, hivi karibuni hautakuwa wakati wa kujenga nyumba? Mji huu ni chungu cha kupikia, nasi ndio nyama.’ 4 Kwa hiyo toa unabii dhidi yao, tabiri, Ewe mwanadamu.”

5 Kisha Roho wa Bwana akaja juu yangu, naye akaniambia niseme: “Hili ndilo Bwana asemalo: Hili ndilo ninyi mnalosema, ee nyumba ya Israeli, lakini ninajua mnalowaza mioyoni mwenu. 6 Mmewaua watu wengi katika mji huu na kujaza barabara zake maiti.

7 “Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi: maiti ulizozitupa huko ni nyama na mji huu ni chungu, lakini nitawaondoa mtoke huko. 8 Mnaogopa upanga, nao upanga huo ndio nitakaouleta juu yenu, asema Bwana Mwenyezi. 9 Nitawaondoa mtoke katika mji na kuwatia mikononi mwa wageni nami nitawaadhibu. 10 Mtaanguka kwa upanga, nami nitatimiza hukumu dhidi yenu katika mipaka ya Israeli. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Bwana. 11 Mji huu hautakuwa chungu kwa ajili yenu, wala hamtakuwa nyama ndani yake. Nitatoa hukumu dhidi yenu katika mipaka ya Israeli. 12 Nanyi mtajua ya kuwa Mimi ndimi Bwana, kwa kuwa hamkufuata amri zangu wala kuzishika sheria zangu, bali mmefuata mwenendo wa mataifa yanayowazunguka.”

13 Basi nilipokuwa ninatoa unabii, Pelatia mwana wa Benaya akafa. Ndipo nikaanguka kifudifudi, nikalia kwa sauti kuu nikasema, “Ee Bwana Mwenyezi! Je utaangamiza kabisa mabaki ya Israeli?”

14 Neno la Bwana likanijia kusema: 15 “Mwanadamu, ndugu zako, ndugu zako ambao ni wa uhusiano wa damu na nyumba yote ya Israeli, ndio wale ambao watu wa Yerusalemu wamesema, ‘Wako mbali na Bwana; nchi hii tulipewa sisi kuwa milki yetu.’

16 “Kwa hiyo sema, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Ingawa niliwapeleka mbali miongoni mwa mataifa na kuwatawanya katika nchi mbalimbali, lakini kwa kitambo kidogo mimi nimekuwa mahali patakatifu kwao katika nchi walizokwenda.’

17 “Kwa hiyo sema: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Nitawakusanyeni kutoka mataifa na kuwarudisha kutoka nchi ambazo mmetawanywa, nami nitawarudishia nchi ya Israeli.’

18 “Watairudia nchi na kuondoa vinyago vyote vya upotovu na sanamu zote za machukizo. 19 Nitawapa moyo mmoja na kuweka roho mpya ndani yao, nitaondoa kutoka ndani yao moyo wa jiwe na kuwapa moyo wa nyama. 20 Kisha watafuata amri zangu na kuwa waangalifu kutii sheria zangu. Watakuwa watu wangu nami nitakuwa Mungu wao. 21 Lakini kwa wale ambao mioyo yao imeambatana na vinyago vyao vya upotovu na sanamu zao za machukizo, nitaleta juu ya vichwa vyao yale waliyotenda asema Bwana Mwenyezi.”